Watafiti wafanikiwa kuondoa VVU kwa panya

Miss Zomboko

JF-Expert Member
May 18, 2014
4,501
9,279

*Majaribio yaliyofanywa yafanikiwa kwa asilimia 100

*Mamlaka zikiruhusu, tiba kuanza kutolewa mwakani

NEW YORK- MAREKANI

WATAFITI nchini Marekani wamesema wamefanikiwa kuondoa Virusi Vya Ukimwi kutoka kwenye vinasaba (DNA) vya panya, mafanikio ambayo wanasayansi wanasema yanaweza kuwa hatua ya kwanza kuelekea tiba ngumu ya ugonjwa huo kwa binadamu.

Matokeo ya utafiti huo yaliyotangazwa wiki hii yamethibitishwa na wanasayansi zaidi ya 30 kutoka Vyuo Vikuu vya Temple na kile cha Tiba cha Nebraska.

Mmoja wa watafiti waandamizi aliyeshiriki katika utafiti huo Kamel Khalili wa Chuo Kikuu cha Temple cha nchini Marekani amesema kutokana na mafanikio hayo endapo mamlaka za chakula na dawa zitathibtisha tiba hiyo kwa binadamu inaweza kuanza kutumika mapema mwaka ujao.

Watafiti hao wanasema hatua hiyo imewezekana kwa kuchanganya dawa za kufubaza maambukizi ya virusi na kifaa kinachoitwa CRISPR ambacho kinaweza kubadilisha jeni.

Watafiti hao waliondoa Virusi Vya Ukimwi katika panya 9 kati ya 23 ambao mifumo yao ya kinga ilibadilishwa kulingana na ile ya binadamu.

Khalili na wataalamu wengine wa Virusi Vya Ukimwi wanasisitiza kuwa hatua hiyo ni kubwa kisayansi na matokeo yaliyoonekana kwa panya hao yanatoa mwanga wa tiba hiyo kufanikiwa kwa binadamu.

” Tulijua kile tulichohitaji kufanya, lakini teknolojia haikupatikana,” Khalili aliliambia Washington Post, akisema timu yake ilikuwa ikisubiri nyenzo kama CRISPR ili kukabiliana na virusi.

Khalili alikaririwa na Washington Post akisema matokeo hayo yalikuwa ni ya kushangaza.

Ukimwi ni ugonjwa unaoathiri kinga ya mwili, hivi sasa unaweza kudhibitiwa tu kwa tiba inayojulikana kama ‘antiretroviral’ ambayo inafubaza virusi lakini haitibu.

Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonyesha ugonjwa wa ukimwi umeathiri watu milioni 37 duniani kote.

Kwa mujibu wa takwimu za hivi karibuni kutoka WHO watu milioni 22 ndio wanaotumia dawa hiyo za kufubaza virusi.

WHO inasema karibu watu milioni moja walikufa kwa magonjwa yanayoendana na Ukimwi mwaka 2017.

Mapema mwaka huu, wanasayansi walionya juu ya uthibitisho wa mtu wa pili aliyetangazwa kupona virusi vya ukimwi baada ya yule aliyetangazwa miaka 12 iliyopita, wakisema ilikuwa ni mapema mno kutangaza mtu huyo kupona.

Wagonjwa wote wawili waliotangazwa kupona awali walitibiwa kwa ‘stem cell transplant’, matibabu ambayo watalaamu walisema ni hatari yanaweza kusababisha athari kwa upande mwingine na kuleta madhara makubwa na walionya tiba hiyo kutopelekwa kwa watu wengine wengi.

MATIBABU YA SASA

Awali, kabla hawajafanikiwa kupata tiba kamili, timu ya Khalili huko Temple walibaini njia ya kuondoa Virusi vya Ukimwi kutoka kwenye DNA ya panya haikuweza kuondoa kabisa maambukizi.

Kwa sababu hiyo timu hiyo ya maabara ya Khalili iliunganisha nguvu na timu kutoka Chuo Kikuu cha Tiba Cha Nebraska (UNMC) ili kuangalia njia tofauti ya kushambulia tatizo.

Kwa pamoja wanasayansi hayo walichanganya mbinu ya kubadilisha jeni kwa kutumia dawa iliyotengenezwa kushambulia Virusi Vya Ukimwi iliyotengenezwa na UNMC.

Howard Gendelman kutoka UNMC aliiambia Washington Post kuwa dawa yao ya majaribio imeonekana kufanya kazi kwa muda mrefu zaidi kuliko dawa za kawaida, maana yake ni kwamba inaweza kutumiwa kila miezi michache badala ya kila siku kama zilivyo dawa nyingine zinazotumika sasa.

Kwa sababu hiyo alisema dawa hiyo imeonekana kurahisisha kazi iliyofanywa na timu ya Khalili ya kubadilisha jeni na hivyo kutokomeza Virusi vya Ukimwi.

“Ikiwa unaweza kupunguza kiasi cha virusi ambacho kinaachwa na CRISPR, uwezekano wa CRISPR kuwa na ufanisi zaidi ukiendelea upo,” alisema.

Pamoja na hayo Khalili alisema yeye na timu yake wataweza kufanya majaribio kwa binadamu kwa kutumia dawa za kawaida hata kama zile zilizozalishwa katika maabara ya UNMC hazitaruhusiwa kwa matumizi .

Steven Deeks, Profesa wa Chuo Kikuu cha California kilichoko San Francisco ambaye amefanya kazi sana juu ya ugonjwa wa ukimwi, alisema kutumia njia ya kubadili jeni kuondoa Virusi vya Ukimwi kutoka kwa mnyama aliye hai ni hatua kubwa ya mbele.

Lakini alionya kwamba kutumia njia hiyo kwa binadamu inaweza kuwa na changamoto zaidi.

“Wanasayansi watalazimika kukabiliana na tofauti nyingi za virusi, shida zaidi katika kutoa teknolojia ya kubadili jeni na zaidi uwezekano wa kukata jeni za binadamu wakati wa kujaribu kulenga Virusi Vya Ukimwi,” alisema Deeks ambaye alisisitiza kuwa njia yenyewe iliyogundulika haina shaka isipokuwa utekelezaji wake.

Wakati wanasayansi wakija na taarifa hizo, Dk. Leonard Maboko wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi (Tacaids) akielezea hali ya maambukizi kwa hapa nchini alisema watu milioni 1.4 wanaoishi na ugonjwa huo nchini.

Alipotakiwa kutoa maoni kuhusu utafiti huo mpya, Dk Maboko alilitaka gazeti hili kuwasiliana na Wizara ya Afya kwa kuwa wao ndio wanaoshughulika na tiba na chanjo.

Gazeti hili liliwasiliana na Mganga Mkuu wa Serikali, Profesa Mohammed Kambi lakini alimtaka mwandishi amtumie ujumbe mfupi lakini baadae alipopigiwa hakupatikana.

Walipotafutwa Wizara ya Afya kupitia kwa msemaji wao, Catherine Sungura alisema Waziri, Naibu na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo walikuwa kwenye mkutano.

Catherine alisema kwa uelewa wake tiba hiyo ni hadi pale WHO itakapoidhinisha ndipo nchi nyingine ziweze kutumia.
 
Hizi tafiti hizi, maana juzi tu ilipostiwa story ya namna hii kutoka Kenya. Walete minjingu tu hio watu tupige kavu bila stress za kupima kila saa
 
Ilikuwa ni project ambapo ilitakiwa2025 ukimwi utokomezwe kabisa naona project iko mwishon ndio maana tiba inakuja, walikuwa nayo toka zaman ila walikuwa wanakamilisha mkakati wao
 
UKIMWI ni zimwi lililoumbwa na USA, wataishia kutafiti tu japo tiba wanayo. Suala wanalojiuliza ni Programs na NGOs zilizoanzishwa kwa ajili ya kupambana na kuenea kwa UKIMWI zitakwenda wapi endapo tiba ikipatikana.
Ilikuwa ni project ambapo ilitakiwa2025 ukimwi utokomezwe kabisa naona project iko mwishon ndio maana tiba inakuja, walikuwa nayo toka zaman ila walikuwa wanakamilisha mkakati wao
 
Wanailagai dunia tu virusi vya ukimwi wametengeneza wao! Sasa wanaona watafiti wengi wamechachamaa kuvumbua dawa, wameona bora wawahi kutoa dawa! chelewa chelewa utakuta mwana siyo wako 🤣🤣
 
Wazungu bwana wamesubiri tuwe wengi halafu watoe dawa.wamegundua kondom haziendi watu wametulia .
 
Ilikuwa ni project ambapo ilitakiwa2025 ukimwi utokomezwe kabisa naona project iko mwishon ndio maana tiba inakuja, walikuwa nayo toka zaman ila walikuwa wanakamilisha mkakati wao
Nasikia ilikuwa project ya miaka 50
 
Hizi tafiti hizi, maana juzi tu ilipostiwa story ya namna hii kutoka Kenya. Walete minjingu tu hio watu tupige kavu bila stress za kupima kila saa
Hata hapa kwetu tiba ipo ingawa ni ya miti shamba. Watu kadhaa waliotumia wamepima na majibu kuonesha wamepona. Tatizo linabaki kwa serikali yetu na wizara ya afya kufanyia kazi ugunduzi huu.
Hizi tafiti hizi, maana juzi tu ilipostiwa story ya namna hii kutoka Kenya. Walete minjingu tu hio watu tupige kavu bila stress za kupima kila saa
 
Kila siku naskia dawa imegundulika mara israel mara u.k mara sijui wapi lakini hakuna ambayo iko sokoni
 
Back
Top Bottom